Ufaransa yarudia historia dhidi ya Uruguay

Imeandikwa .

Na Anthony Aroshee

Ijumaa, Julai 6, 2018

Ufaransa imekuwa timu ya kwanza kutinga nusu fainali ya michuano ya kombe la dunia nchini Urusi baada ya kuwachapa Uruguay mabao 2-0 katika mchezo wa robo fainali uliochezwa Ijumaa ya Julai 6 kwenye Uwanja wa Nizhny Novgorod.

Mabingwa hao wa kombe la dunia mwaka 1998 walijipatia mabao hayo kupitia Raphael Varane aliyefunga bao la kwanza dakika ya 40 kabla ya Antoine Griezmann kuhitimisha ushindi huo kwa kupachika bao la pili katika dakika ya 61 mabao yaliyoiwezesha Ufaransa kusonga mbele.

Kufuatia matokeo hayo, timu ya taifa ya Ufaransa Les Blues imefanikiwa kuweka historia nyingine dhidi ya Uruguay katika Michuano ya kombe la dunia.
Katika kukutana kwao Ufaransa imeifunga Uruguay mara mbili ikipoteza mechi moja na kutoka sare mara saba.

Kwenye michuano ya kombe la dunia pekee timu hizo zimekutana mara tatu wakati zikitoka sare mara mbili katika kukutana huko ikiwa ni mwaka 2010 nchini Afrika Kusini na 2002 nchini Korea Kusini na Japan huku ikishinda mchezo huo mmoja mwaka 1966 nchini England.

Uruguay imetwaa Kombe la Dunia mara mbili mwaka 1930 ikiwa yenyeji na 1950 katika michuano iliyoandaliwa nchini Brazil.

Chapa